Magonjwa ya kuku ni maradhi yanayoathiri afya ya kuku na kusumbua wafugaji wengi wa kuku, hasa wafugaji wadogowadogo.
Kuku, kama walivyo viumbehai wengine, hupatwa na magonjwa mbalimbali. Kwa kuwa kuku ni mifugo ya binadamu, hivyo ni jukumu la mfugaji kutatua tatizo linapotokea ambalo hujumuisha afya ya mfugo wake – kuku.
Makala hii inaelezea baadhi ya magonjwa ya kuku yanayowakabili wafugaji wengi na baadhi ya njia za kupunguza au kujilinda na magonjwa haya
Ugonjwa huu huathiri kuku katika umri wowote na unapoingia kwenye kundi huweza kuua idadi kubwa ya kuku hao hadi kufikia asilimia tisini. Ndege wakubwa hustahimili kidogo kuliko wale wadogo kwasababu ya usugu mwilini (body immunity) uliojengeka kwa muda mrefu zaidi.
. Ugonjwa huu husababishwa na kimelea cha kirusi kiitwacho Paramyxo viridae na huenezwa kwa njia ya hewa na kugusana.
Dalili zake:
• Kukohoa na kuhema kwa shida
• Ute hutoka mdomoni na puani
• Kuku walioathirika hupata kizunguzungu.
• Kuharisha uharo wa kijani na njano
• Kuzubaa, kusinzia na mabawa kushuka
• Baada ya siku 2 kuku hupindisha shingo
• Kuvimba macho
• Kuzunguka
• Kuku hutaga mayai hafifu.
• 90% ya kuku huweza kufa
Tiba:
Ugonjwa huu hauna dawa.
Kinga:
• Kuchanja, chanja kuku wako kila baada ya miezi mitatu na mara nne kwa mwaka.
2. Kuharisha Damu (Coccidiosis):
Ugonjwa huu husababishwa na kimelea cha protozoa cha jamii ya Eimeria (Eimeria tenela, Eimeriamaxima, na Eimeria acervulina)
Kwa kawaida wadudu hawa hupenda kuishi kwenye mazingira machafu, kama vinyesi, vyakula vilivyooza na umaji maji.(moist environments).
Dalili zake:
• Kinyesi cha kuku huchanganyika na damu
• Wakati mwingine kuku hunya damu.
• Kuku hudhoofika sana.
• Kuku huteremsha mabawa yake.
• Hatimaye vifo hutokea.
Tiba;
Ugonjwa huu hutibika kwa kutumia dawa za
(i) Kundi la suphur
Mfano: sulphonamides (ESB3) kwa siku 3-4
(ii) Amprolium
Kinga: Zingatia usafi mara kwa mara
Kwakuwa ugonjwa huu huambatana na majimaji na uchafu wenye vimelea vya ugonjwa huu, ni vizuri kuhakikisha banda la kuku linakuwa safi na kavu wakati wote.
• Tenga kuku wagonjwa kutoka kwa walio wazima.
• Tumia dawa ya kinga ili kuepusha uwezekano wa kuku kuambukizwa ugonjwa huu
Dawa inayopendekezwa ni zile zinzoitwa (coccidiostat).
• Tenga kuku wadogo (vifaranga) kutoka kwenye kundi la wakubwa.
3. Homa ya Matumbo(fowl typhoid):
Husababishwa na vimelea vya wadudu wa bakteria wa jamii ya Salmonella.
Kimelea hicho cha bacteria huitwa Salmonella gallinarum.
Dalili zake:
• Uharo mweupe au wa kijani
• Vifo hufikia kiasi cha 50%
• Rangi ya minofu hugeuka kuwa ya njano
• Viungo vya ndani kama maini, figo, bandama huvimba
• Maini hung’aa kwenye mwanga mkali.
Tiba
Tumia dawa za antibiotiki kama vile furazolidone ili kutibu ugonjwa huu.
KINGA:
• Chanja kuku wako mara kwa mara .
• Fanya usafi wa banda na vyombo vya kulishia na kunyweshea maji ipasavyo.
• Ugonjwa wa mafua ya ndege ni ugonjwa hatari sana kwa kuku na jamii nyingine za ndege.
• Pia ugonjwa huweza kuambukizwa na kusababisha vifo kwa binadamu.
• Ugonjwa huu husababishwa na kirusi kiitwacho Orthomyxo virus.
• Ugonjwa huu huenezwa kwa njia ya kugusana baina ya ndege na ndege na baina ya ndege na binadamu.
Dalili zake:
Dalili za ugonjwa huu huanza kuonekana katika kipindi cha siku 3-7 baada ya kuku kuambukizwa.
Dalili hutofautiana kutokana na umri wa ndege.
Baadhi ya dalili zake ni hizi zifuatazo
• Kuku /ndege hupumua kwa shida (dyspnoea).
• Kuzubaa.
• Kutokwa na machozi.
• Kukohoa na kupiga chafya.
• Kuharisha kinyesi chenye majimaji.
• Sehemu za kichwa zisizo na manyoya huvimba,uvimbe wenye majimaji huonekana kichwani na shingoni.
• Sehemu ya juu kichwani hubadilika na kuwa na rangi ya bluu iliyopauka.
• Kuku hutaga mayai yenye maganda laini.
Tiba:
Ugonjwa huu hauna tiba .
Kinga na kuzuia kuenea kwa ugonjwa huu:
• Toa taarifa kwa mganga (daktari wa mifugo aliye karibu ukiona dalili za ugonjwa huu.
• Tenga mabanda ya kuku wagonjwa na walio wazima.
• Fungia kuku wako wasitembee holela.
• Acha kununua kuku kutoka eneo linalohisiwa kuwa na ugonjwa huu.
• Acha kusafirisha mifugo /ndege bila idhini ya daktari.
• Zuia wageni kutembelea mabanda yako ya kuku.
• Acha kuhamisha mbolea ya kuku kwenda shambani kutoka kwenye banda la kuku wanaoumwa ugonjwa huu.
• Safisha mabanda na kuweka dawa chini ya usimamizi wa mtaalamu wa mifugo na kulipumzisha kwa siku 21kabla ya kuanza kufuga tena.
• Choma moto mkali au fukia chini mbolea kutoka kwenye banda la kuku wanaoumwa ugonjwa huu.
• Pata ushauri kutoka kwa mtaalamu wa mifugo aliye karibu nawe.
5. Gumboro (infectious Bursal Disease):
Ugonjwa huu husababishwa na kirusi
Dalili zake:
• Hushambulia vifaranga
• Uharo mweupe
• Kuchafuka (dirting of anal area)
• Kuvimba
• Kiwango kikubwa cha vifo
• Damu hutapakaa eneo la kutolea kinyesi
Kinga:
• Usafi
• lishe bora
• chanja vifaranga wakiwa na umri wa wiki tatu kwa kutumia chanjo hai (live vaccine)
Ugonjwa wa ndui ya kuku mara nyingi huwashambulia kuku wadogo na wakubwa. Ugonjwa hu husababishwa na virusi.
Jinsi unavyoambukizwa:
• Ugonjwa huu huambukizwa kwa kupitia kwenye vijeraha vya kuku.
• Mbu na wadudu wengine waumao huweza kuambukiza anapomuuma kuku mgonjwa na halafu akamuuma kuku asiye na ugonjwa.
Dalili zake:
• Homa kali.
• Kupoteza hamu ya kula.
• Kupoteza uzito.
• Kutokea kwa vipele sehemu mbalimbali zisizo na manyoya.
• Baada ya siku kati ya 7 hadi 14 vipele hupasuka na kuacha vidonda.
• Vifo huweza kutokea kwa kuku wenye umri mdogo.
• Kutoa kamasi kwenye pua.
• Mara nyingi vipele husababisha kuziba macho.
Matibabu:
Ugonjwa huu hauna tiba,kwani huambukizwa na virus.Ila inashauriwa kuwapa kuku dawa ya Antibiotic ili kuzuia kutibu magonjwa nyemelezi yanayoweza kuwashambulia kuku kupitia kwenye vidonda.
Kinga:
• Ndui ya kuku huzuiwa kwa chanjo ya sindano.
• Vifaranga wapatiwe chanjo wakiwa na umri wa siku moja na kurudiwa baada ya miezi 2 hadi 3.
• Tenga kuku wagonjwa na wazima.
• Epuka madimbwi karibu na nyumba ili kuepusha mazalia ya mbu.
Muhimu:Ili kupunguza kasi endapo ugonjwa huu umewapata kuku,sugua majeraha au vipele kwa pamba iliyochovywa kwenye dawa ya madini joto (Iodine) na baadaye paka mafuta mazito (Petroleum jelly)au samli.Hii sio kutibu ugonjwa bali unawasaidia kuku kulainisha ngozi na macho yapate kuona chakula na maji.
7. Kifua Kikuu cha Ndege(Avian Tuberculosis-TB):
Husababishwa na kimelea aitwaye Mycobacterium avium.
Dalili zake:
• Kukonda na Kupungua uzito
• Vidonda kwenye kishungi
• Kupungua uzito/kukonda
• Kuhara
Kinga:
• Usafi, fanya usafi na vyombo, banda na mazingira .
8. Magonjwa yatokanayo na Lishe (Nutritional and Metabolic Disorders):
Dalili za magonjwa haya hutegemea aina ya virutubisho vinavyokosekana mwilini
Kwa mfano:
• Kupinda miguu (rickets) husababishwa na upungufu wa Vitamin D, madini ya calcium na fosforasi.
• Vidonda vyenye vyenye damu husababishwa na vitamin K
• Kichaa cha kuku na kusinyaa kwa misuli husababishwa na upungufu wa Vitamin E
• Magamba ya Mayai (egg shell)kuwa laini ama umbo kuwa bovu husababishwa na upungufu wa madini ya calcium na fosforasi.
• Kudonoana kusababishwa kwa njia moja au nyingine na upungufu wa chakula na madini ya chuma, fosforasi na calcium
• Kuvimba macho, upungufu wa damu huletwa na upungufu wa vitamin A.
Kinga:
• Kuwapa kuku mlo kamili
• Kuelewa kwa kina aina za chakula kwa kila rika na aina ya kuku ; vifaranga , kuku wa mayai na wa nyama. (Poultry age and classes i.e chicks, layers and broilers)
• Kufanya uchunguzi wa virutubisho vilivyomo katika aina ya chakula unachotumia.
Minyoo iko ya aina tatu kama vile minyoo kamba, minyoo bapa na minyoo ya mviringo
Dalili zake:
• Kudumaa
• Kuwa manyoya hafifu
• Kupungua uzito
• Kukonda
• Minyoo huonekana kwenye kinyesi
Kinga na kuzuia:
USAFI:
• Fanya usafi wa vyombo, banda na mazingira.
• Tenga vifaranga kutoka kwa wale wakubwa.
• Badilisha matandazo kuondoa mazalia ya minyoo.
• Badilisha matandazo kila baada ya miezi mitatu.
TIBA:
• Tumia dawa zinazopendekezwa na wataalamu hasa zile zinazoua minyoo ya aina zote (mfano: piperazine citrate).
• Hakikisha kila baada ya miezi mitatu unawapa kuku wako dawa za minyoo.
10. Kupe, Utitiri, Chawa na Viroboto
Kupe laini waitwao Argus persicus, chawa na viroboto wanaong’ata .
Dalili zake:
• Kujikung’uta.
• Kupiga kelele.
• Kiasi cha damu hupungua mwilini.
• Utando wa ngozi ndani ya kope za macho hupauka.
• Utando wa ngozi ya juu mwilini huwa mnene.
• Magamba ya unga-unga hudondoka.
Kuzuia:
• Tupa au choma masalia ya mayai yasiyoanguliwa na magamba ya mayai yaliyoanguliwa vifaranga.
• Safisha banda mara kwa mara na kunyunyizia dawa; kuna dawa zinazopendekezwa na wataalamu za kunyunyizia kwenye banda la kuku. Mfano wa hizo dawa ni sevin , akheri powder n.k (Dawa hizi ni za unga).
………………………………………………………………………..