Mnyama mgonjwa hutambulika kwa dalili kuu zifuatazo:
Badiliko la tabia – Mnyama mgonjwa hana uchangamfu. Wanyama wengine huwa wakali hawapendi kusogelewa, hulia ovyo ovyo. Kama ni mbwa hubweka kupita kiasi.
Mwenendo – Kutembea bila mpangilio, kupenda kulala chini, kulala chini bila kuamka, huchechemea au kuvuta miguu, kukimbia ovyo bila kufukuzwa
ZIJUE DALILI ZA MNYAMA MGONJWA
Hali ya mwili – Kudhoofu/Kukosa nguvu, Kukonda: mbavu, mifupa kuonekana, manyoya kunyooka au kusimama.
Ulaji wa chakula – Kupungua kwa hamu ya kula, Kutotaka kula kabisa (Anorexia) Kula vitu visivyo vya kawaida, kama mifupa, udongo, manyoya (Kuku) watoto wadogo. Kutapika mara kwa mara, Kunywa maji kidogo au mengi sana
Hali ya uzalishaji – Utoaji wa maziwa kupungua, utagaji wa mayai kupungua.
Hali ya kukua – kasi ya kukua hupungua/hudumaa
Hali ya uzazi – Kutupa mimba, kutoonyesha dalili za joto, kutoshika mimba, kushindwa kupanda (dume), kushindwa kusukuma kondo la nyuma, kuzaa mtoto mfu
Hali ya upumuaji – Kuhema sana, kupumua kwa taabu, kukohoa kwa taabu, kupiga chafya, kutokwa makamasi puani, mdomo kubaki wazi, sauti yenye mikwaruzo, kukoroma mara kwa mara.
Mapigo ya moyo – Kwenda haraka, kwenda polepole, mapigo ya moyo bila mpangilio mzuri, hatimaye kusimama.
Msukumo wa damu – Mwendo wa harakaharaka, mwendo wa pole pole, mwendo uliopooza.
Hali ya kinyesi – Uharo laini, kinyesi kigumu, kinyesi kilichanganyika na damu, kamasi, au minyoo, kutoa kinyesi mara nyingi
Hali ya mkojo – Kukojoa damu, mkojo wa rangi ya njano, mkojo mweupe sana, kukojoa mara nyingi,
Hali ya joto la mwili – Homa: joto la mwili hupanda kuliko kawaida.
Umauti – Joto la mwili kuwa chini ya lile la kawaida, Joto la mwili kawaida: Ng,ombe, ngamia, farasi: 38.5oC, mbuzi, kondoo, kuku: 40oC. mbwa na paka huwa 39oC, binadamu 37oC.
Hali ya viungo mbalimbali: – Ngozi: Kutokea vidonda, upele, uvimbe majipu ukosefu wa nywele au manyoya
Mdomo: mapovu, kuchuruzika mate, kuumwa meno.
Macho: machozi kutoa usaa au ute kubadilika rangi na kutoona.
Kiwele: kuvimba, kutotoa maziwa au maziwa kuganda.
Mkia: kunyooka, kutoweza kupindapinda kufukuza inzi,
Tumbo: kuvimba kuliko kawaida.
Uke: kuvimba sana au kutoa uchafu uume (penis): kuvimba sana au kutoa uchafu, masikio:kutoa uchafu/usaa
MAJUKUMU YA MFUGAJI
Mfugaji anaweza kulinda vizuri afya ya mifugo yake kama atazingatia mambo makuu yafuatayo:
– Kutambua mapema dalili za ugonjwa.
– Kupeleka habari kwa mtaalamu wa mifugo ili aweze kutoa tiba sahihi.
– Kujua vizuri dawa za kinga na tiba ya maradhi ya mifugo na jinsi ya kuyakabili.
– Kutunza usafi wamazingira, vyombo, wahudumu, chakula na maji.
– Kutilia maanani ushauri na maelekezo ya wataalamu.
…………………………………………………………………………………………………………..