Mambo yanayomfanya mfugaji kuamua atumie njia fulani ya kufuga ni pamoja na uwezo wa kugharamia shughuli ya ufugaji wa kuku na ukubwa wa eneo alilonalo la kufugia. Katika sehemu hii utajifunza njia tatu za kufuga kuku ambazo ni:
1. Kufuga huria
Kuku huachwa wenyewe kujitafutia chakula na maji. Njia hii inatumika zaidi kufuga kuku wa kienyeji. Mara chache sana mfugaji huwapatia kuku chakula cha ziada. Kwa ufugaji huu lazima kuwe na eneo kubwa la kutosha kuku kuzunguka na kutafuta chakula. Kuku hulala eneo lisilo rasmi kama vile jikoni, kwenye kiambata n.k.
Faida zake
• Ni njia rahisi ya kufuga.
• Gharama yake pia ni ndogo.
• Kuku wanapata mazoezi ya kutosha.
• Kuku wanapata chakula mchanganyiko ambacho kinafaa kiafya.
Hasara zake
• Kuku huwa hatarini kuibiwa au kudhurika na wanyama wakali na hali mbaya ya hewa.
• Ukuaji wa kuku ni hafifu, hufikia uzito wa kilo 1.2 baada ya mwaka.
• Huharibu mazingira kama kula na mimea ya bustanini mazao kama nafaka.
• Ni rahisi kuambukizwa magonjwa.
2. Kufuga nusu ndani – nusu nje
Huu ni mtindo wa kufuga ambapo kuku wanakuwa na banda lililounganishwana uzio kwa upande wa mbele. Hapa kuku wanaweza kushinda ndani ya banda au nje ya banda wakiwa ndani ya uzio. Wakati wa mchana kuku huwa huru kushinda ndani ya banda hasa wanapotaka kutaga na wakati wa kuatamia au wanaweza kukaa ndani ya uzio nje.
Faida za kufuga nusu ndani na nusu nje
• Kuku wanakuwa salama mbali na maadui mbali mbali.
• Utaweza kuwalisha kuku wako vizuri hivyo wataweza kuongeza uzalishaji wa mayai na wa nyama (kwa kukua haraka).• Itakuwa rahisi kwako kudhibiti wadudu na vimelea vinavyoweza kuleta magonjwa kwa kuku wako.
• Ni rahisi kuwatenganisha kuku katika makundi tofauti na kuwahudumia ipasavyo.
• Ni rahisi kutambua kuku wagonjwa kuliko kufuga huria.
• Kuku watapata mwanga wa jua wa kutosha pamoja na hewa safi.Wakati wa jua kali watakuwa huru kuingia ndani ya banda na kukaa kivulini.
• Kuku hawatafanya huharibifu wa mazao yako shambani au bustanini na kwa majirani zako.
• Utapata urahisi wa kukusanya na kupeleka mbolea bustanini au shambani.
Changamoto ya kufuga nusu ndani na nusu nje
• Huna budi uwe na muda wa kutosha kwa ajili ya kuwahudumia kuku wako.
• Pia utahitaji kuwa na eneo kubwa kiasi la kufugia.
• Pia utaingia gharama ya ziada kidogo ya kutengeneza banda na wigo na kuwapatia uku chakula cha ziada.
• Hata hivyo gharama za muda huo na za vifaa vingine zitafidiwa na mapato ya ziada utakayopata kwa kufuga kwa njia hii.
Njia nyingine ni kuwafuga kuku ndani tu. Katika njia hii, kuku hukaa ndani wakati wote. Njia hii ya ufugaji utumiwa zaidi na wafugaji wa kuku wa kisasa. Lakini yaweza kutumika hata kwa kuku wa asili hasa katika sehemu zenye ufinyu wa maeneo.
Faida za kufuga ndani tu
• Ni rahisi kutambua na kudhibiti magonjwa.
• Ni rahisi kudhibiti upotevu wa kuku, mayai na vifaranga.
• Ni rahisi kuwapatia chakula kulingana na mahitaji ya kila kundi.
• Ni rahisi kuwatambua na kuwaondoa kuku wasiozalisha katika kundi.
Changamoto za ufugaji wa ndani ya banda tu
• Unatakiwa uwe na muda wa kutosha wa kuwahudumia kuku wako kikamilifu.
• Pia unatakiwa kuwa na mtaji mkubwa wa kujenga banda na kuwanunulia kuku chakula.
• Ugonjwa ukiingia na rahisi kuambukizana.Vilevile kuku huweza kuanza tabia mbaya kama kudonoana, n.k.
Ni ufugaji upi unafaa zaidi kutumika kwenye mazingira ya vijijini?
Kwa ujumla, njia rahisi na inayopendekezwa kutumiwa na mfugaji wa kawaida kijijini ni ya ufugaji wa nusu ndani na nusu nje, yaani nusu huria. Hii inatokana na faida zake kama zilizoainishwa hapo awali. Kwa kutumia mfumo huu wa ufugaji, utaepuka hasara za kufuga kwa mtindo wa huria kama zilivyainishwa mwanzoni mwa sehemu hii ya kitabu hiki.
Pia ukitumia mtindo wa ufugaji wa nusu huria utafanya ufugaji wako kwa njia bora zaidi ndani ya uwezo ulionao, kwa sababu kwa sehemu kubwa utatumia mali ghafi inayopatikana katika eneo lako………………………………………………………