UTANGULIZI
Kabla hujaamua kufuga sungura hakikisha ya kwamba umejitoa na una muda wa kuwahudumia wanyama waha, ufugaji wao si rahisi kama vile ukifuga paka au mbwa, sungura wanahitaji uangalizi na hasa kwenye usafi kwa sababu ni rahisi kwao kupata maradhi yatokanayo na mazingira mabaya na machafu.
MABANDA
Kuna aina mbili za mabanda ya kufugia kwanza ni yale ya kuwafungia ndani muda wote bila kutoka nje na ya pili ni ile ya pili ni nusu nusu yaani wanakuwa na mabanda na wanaweza kutoka nje kwenye ua maalum, katika aina zote mbili ni muhimu kuhakikisha hakuna upenyo wa kuruhusu panya kupita kwa sababu huwa wanakula watoto wa sungura.
UFUGAJI WA NDANI
1 – Usitumie banda la kioo (aquarium) kwa sababu halina hewa ya kutosha na ni vigumu kusafisha
2 – Sakafu ya nyavu za waya ni nzuri zaidi ila hakikisha hakuna sehemu zenye ncha kali inayoweza kuwaumiza sungura, kwani wakumia ni mpaka wapone wenyewe au umchinje kwa sababu ukitumia dawa za antibiotic sungura hana uwezo wa kuzimeng’enya na kuisha mwilini mwake, siku ukimchinja atabakia na dawa na hata ukinusa nyama yake utahisi harufu ya dawa
3 – Ukubwa wa banda usipungue mita 4 * 2 kwa kila sungura mmoja, likiwa kubwa zaidi ni vizuri
4 – Chini kuwekewe matandazio kama nyasi kavu au maranda ya mbao, lakini maranda yatokanbayo na miti yenye mafuta kama mi-pine na mikaratusi hayafai, wawekee kipande cha blanket au taulo la zamani kwa ajili ya kulalia na kujifungulia hasa kwa wazazi
5 – Ni muhimu kuwawekea sehemu ya kujificha mara wanapohisi hatari, unaweza kutumia mbao, box gumu au plastiki.
UFUGAJI HURIA
1 – Sehemu yote izungushiwe wavu wa kuku kuzuia panya kuingia na wanyama wengine kama paka, mbwa, mwewe nk
2 – Upande mmoja uwe na mabanda, sehemu ya chakula na maji pamoja na kivuli kwa ajili ya sungura kupumzika
3 – Futi moja chini ya udongo kuwe na zege kuzuia sungura kuchimba na kwenda mbali
4 – Eneo la wazi liwe huru na hatari zote za sumu kama dawa za kuulia wadudu au mbolea, pia majani yaliyoota yasiwe ni yale yenye sumu (waone wataalamu wakushauri au ng’oa yote)
MAJI
Tumia mabakuli ya kigae, plastiki au jengea kwa saruji, maji yabadilishwe kila siku na vyombo visafishwe kila siku
CHAKULA
Wapewe majani, mabaki ya mboga za jikoni baada ya kuchambuliwa, pia unaweza kuwawekea pumba au chakula cha kuku (growers mash) kwenye vyombo maalum kama chakula chenye virutubisho (concentrates)
USAFI
Kila siku jaribu kuondoa uchafu kama vyakula vilivyo mwagika, na kinyesi kilichoganda kwenya matandazio, fagia na kubadili matandazio angalau mara moja kwa wiki, manyoya ya sungura mzazi yasiondolewe hii huonyesha kwamba anakaribia kujifungua watoto
MENO
Wakati mwingine meno ya mbele hukua sana na kumsababishia usumbufu wakati wa kula, waone wataalam ukiona ni marefu zaidi na yanahitaji kupunguzwa, dalili kuu ni sungura kushindwa kula kwa zaidi ya masaa 12
MIGUU
Miguu ya sungura si kama ya wanyama wengine, nyayo zake zimefunikwa kwa manyoya, angalia ukiona yananyonyoka kuna tatizo chunguza, kucha zake nazi huhitaji kupunguzwa zikikua sana
UBEBAJI
Usimbebe kwa kutumia masiki yake huwa wanaumia sana, shika ngozi nyuma ya shingo kama paka ukitaka kumbeba
DAWA
Wapewe dawa ya minyoo kama piperazine kila baada ya miezi mitatu, dawa za wadudu kama akheri powdeer zinyunyuziwe kwenya mabanda yao kuzuia viroboto, usiwape dawa nyingine bila ushauri wa kitaalamu, antibiotics ndio usijaribu kabisa kama nilivyosema mwanzo
Baada ya kujua jinsi ya kufuga Sungura kuna watu wanasema ,sungura hawawezi kuliwa? lakini mbona watu wanafanya biashara ya kuuza sungura wa nyama.