Yaweza kutokea baadhi ya kuku wakawa watagaji wazuri wa mayai lakini hawapendi kuatamia. Katika hali hiyo ni vyema wakachaguliwa kuku (mitetea) wengine ili kuatamia mayai yao kwa uanguaji mzuri.
UTARATIBU UFUATAO UTATUMIKA
Tafuta mtetea aliyefikia umri wa kutaga au kuku aliyekwishawahi kutotoa.
Tafuta mawe matatu ya mviringo au viazi mbatata vya ukubwa wa yai au vibao vilivyochongwa kwa umbile la yai au mayai yasiyo na mbegu (mayai viza, au ya kuku wa kisasa).
Muwekee kuku huyo mayai bandia yasiyopungua matatu kwenye kiota wakati wa usiku na umfungie humo usiku kucha hadi asubuhi na ukimuona anaendelea kuatamia basi usiku unaofuata toa mayai bandia na umuwekee mayai halisi.
Weka mayai kwenye kiota huku mikono yako ikiwa imepakwa majivu ili kuepuka kuwa na harufu kwani kuku anaweza kuyasusa.
KUWATAYARISHA KUKU WA KUATAMIA
Kuku wanaotazamiwa kuatamia ni lazima wachunguzwe kwa makini kabla ya kuatamia ili kuhakikisha kwamba hawana chawa, utitiri au viroboto.
Kuwepo kwa wadudu hao kutawafanya kuku wakose raha na wasitulie kwenye viota vyao, matokeo yake ni kuanguliwa kwa vifaranga wachache.
Ili kuua au kuzuia wadudu hawa, fanya yafuatayo:
1.Toa matandiko (litter) ndani ya banda.
2.Nyunyiza dawa ya kuua wadudu (viroboto, utitiri nk.) ndani ya kiota.
3.Pia mnyunyizie dawa kuku anayetarajiwa kuatamia au fanyia farmigation banda zima kabla ya kuingiza kuku.
SIFA ZA KIOTA NA CHUMBA CHA KUATAMIA
Kuku wanao atamia watengwe katika chumba ili kuondoa tatizo la kutagiana.
Mlango na dirisha viwekwe wavu ili muda wa mchana mwanga na hewa uweze kuingia ndani.
Chumba kiwe na nafasi ya kutosha kuweka viota, vyombo vya chakula na maji.
Ili kutumia eneo vizuri viota vinaweza kutengenezwa ukutani kama mashelfu.
Viota viundwe vizuri kwa nyasi, maranda makavu ya mbao, au nguo ya pamba lakini isiyo tetroni.
Viota visiwe sehemu yenye unyevunyevu. Idadi ya viota vilingane na idadi ya matetea walio chaguliwa KUATAMIWA
…………………………………………………………………………………………………………………