HATUA ZA KULEA VIFARANGA (new) I Mshindo Media

Habari ya uzima ndugu mfugaji!

Huu ni mwanzo wa somo la kulea vifaranga , tutajifunza ujenzi wa banda la vifaranga, vitu vya muhimu katika banda la vifaranga, kujiandaa kupokea vifaranga, chanjo na dawa, sababu za vifo kwa vifaranga , lishe bora kwa vifaranga, na jinsi ya kudhibiti vifo nk.

Mwanzo huu ,sehemu ya kwanza tutajifunza ujenzi wa banda la vifaranga/ vitu vya muhimu katika banda la vifaranga.

Nyumba Ya Kulelea Vifaranga

Ukipenda kujenga nyumba ya vifaranga itafaa ujue  yafuatayo:- 

_ Nyumba ya vifaranga iwe karibu na nyumba yako mwenyewe ili uweze kuwakagua vifaranga wako mara kwa mara. 

_Ijengwe hatua 20 au zaidi mbali na nyumba ya kuku wakubwa, hii ni kinga mojawapo ya kupunguza hatari ya maambukizi ya magonjwa. 

_Nyumba ya vifaranga isiruhusu ubaridi au unyevu au wanyama waharibifu kuingia. 

#Lakini nyumba iingize hewa na mwanga wa kutosha kila wakati. 

_ Nyumba iwe na eneo la kutosha ili vifaranga wapate nafasi ya kutembea kutafuta chakula na maji bila kubanana. 

_Ijengwe kwenye sehemu isiyoelekea upepo unaotoka kwenye nyumba ya kuku wakubwa.

✅ Tahadhari hii husaidia vifaranga kuepukana na magonjwa yanayoenezwa na upepo. 

Ukubwa wa Nyumba 

Eneo:

Vifaranga hawahitaji eneo kubwa katika muda wa majuma 4 ya kwanza. Nafasi inayohitajiwa kwa kukadiria ni meta za eneo 1 kwa kila vifaranga 16. Kwa mfano nyumba yenye meta 10 za mraba inatosha kulea vifaranga 160 hadi umri wa majuma 4.

 Vipimo vya nyumba yenye eneo kama hili inaweza kuwa na hatua 5 kwa hatua 4 au hatua 3 kwa 3.25. Utajenga kutegemea na eneo ulilonalo. Baada ya majuma 4 ya umri ongeza nafasi na uwape vifaranga eneo la kuwatosha. 

✅ Zingatia ukubwa wa nyumba inategemea na umri /aina ya kuku

Sakafu:

Sakafu nzuri katika nyumba ya vifaranga ikiwezekana inafaa ijengwe na simenti iliochanganywa na zege.

Ili kupunguza gharama, unaweza kutumia vifaa vya ujenzi

vinavyopatikana kirahisi katika eneo lako vitumikavyo kusiriba sakafu kama udongo wa

kichuguu.

Ukuta:

Ingefaa kuta za nyumba za kulea vifaranga ziwe za matofali, udongo, mabati au debe. 

Kuta za matofari na udongo zipigwe lipu ili kurahisisha usafi shaji wa nyumba au umwagiaji wa dawa. Urefu wa kuta uwe tangu meta 1.8 – 2.4 (futi 6-8). Sehemu ya kutoka chini ya meta 0.9 – 1.2 (futi 3 – 4) izibwe na ukuta wa tofali au udongo na sehemu ya juu iliyobakia yenye meta 0.9 – 1.2 (futi) 3-4) ijengwe kwa wavu wa chuma au fito. 

Mbao:

 Nguzo za miti au mbao zilowekwe dawa ya mbao kama vile “Dudu killer” au oili chafu ili kuzuia kuoza. Ukitumia miti ni vizuri uondoe magome ambayo yanaweza kuweka vimelea na wadudu.

Madirisha:

Unaweza kutumia maboksi, mikeka ya magunia, mapazia ya magunia ni rahisi na

yanaweza kuwekwa kwa kupigiliwa misumari kwenye dari na upande wa chini pazia ipigiliwe misumari kwenye ubao ili ininginie.Unaweza kukunja mapazia/magunia ili uingize hewa na mwanga wa kutosha katika nyumba ya vifaranga. ( hii inategemea na mazingira ulipo na jinsi utakavyo penda)

Paa:

Mjengo wa paa uwe unaoweza kuwapatia vifaranga hewa ya kutosha hivyo paa liwe na tundu la kutoa nje hewa yenye joto.

 Kwa kadri utakavyoweza, unaweza kutumia madebe,

mabati, makuti au nyasi n.k. kuezeka nyumba ya vifaranga. 

#Sehemu ya paa ikianza kuvuja iezekwe bila kuchelewa.

✅Tambua banda bora litaepusha vifaranga wako na magonjwa, pia litaepusha vifaranga wako na wadudu hatarishi

✅Katika Ufugaji Kuku Kitu cha kwanza ni ujenzi wa banda hatua hii huwa ni hatua ya mwanzo nani ngumu pia , ukishakamilisha banda bora hapo ndio ufugaji huanza.

 Jenga banda bora kwaajili ya kuku wako! Banda bora mifugo bora zaidi

VITU VYA MUHIMU KATIKA BANDA LA VIFARANGA.

Vitu Vya Muhimu Katika Banda La Vifaranga:

1.Bruda/brooder

Kifaa hiki Mara nyingi huwa ni cha duara ,Hii ni kwasababu ya kuzuia Vifaranga visikusanyike pembeni. Unaweza tengeneza bruda kwa kutumia mbao, singbod,box nk

Katika kulea Vifaranga kitu  mojawapo ambacho ni cha muhimu ni jinsi ya kuwapatia joto

Umuhimu Wa Bruda Kwa Vifaranga

Mfugaji anaetumia bruda na yule asiye tumia bruda wana utofauti Mkubwa:

_Kwanza ukitumia bruda jinsi ya kufanya usafi ni rahisi kwasababu Vifaranga huwa kwenye eneo lile la bruda na kama wanapo chafua huo uchafu hauwezi sambaa banda zima.

_Ukitumia bruda utapata urahisi wa kuhakikisha Vifaranga wako wana pata joto la kutosha, kwasababu kama Vifaranga wapo kwenye bruda na umewafungia taa ile joto ya taa itaenda moja kwa moja kwenye Vifaranga halisambai ovyo.

_Kwa kuwa joto halisambai ovyo Basi kuna uwezekano wa kutumia vyanzo vichache vya joto tofauti na yule asiye tumia bruda.

_Kama utatumia umeme , mkaa au Mafuta katika kuwapatia joto Vifaranga, utakapo tumia bruda cost itapungua kwasababu joto litawahi kuwatosheleza Vifaranga.

“”Tofauti na yule asietumia bruda na kuweka balbu nyingi ili Vifaranga wapate joto.””

Kwa kuwa Vifaranga wanapata joto vizuri basi utafanikiwa kupunguza vifo kwa Vifaranga wako.

Vitu Vitakavyo Kuwa Ndani Ya Bruda

• Vyombo vya maji

• Vyombo vya chakula

• Chanzo cha joto unaweza tumia

• Balbu

•Jiko la mkaa: Jiko la mkaa linaweza kutumika badala ya taa kwa ajili ya kuwapa vifaranga joto. Unapotumia

jiko la mkaa ni hakikisha kwamba mkaa unaotumia hautoi moshi na chumba kinapitisha

hewa safi na ya kutosha. Pia jiko liwekwe juu ya matofaili ili kuzuia vifaranga wasiliguse. (Hakikisha unaliwashia nje ya banda)

• Chemli

•Vyungu.

2. Vyombo vya chakula

Ili vifaranga wakue vizuri vyombo vya

chakula lazima viwafae. Vipimo pamoja na

idadi ya vyombo vya chakula ni vya muhimu

viwatosheleze.

Chombo chenye urefu wa (futi

3 x inch 3) kinatosha vifaranga 100. Ukitumia

mbao kutengeneza vyombo vya chakula

unashauriwa mbao ziwe unene wa cm 1/25

(inchi ½). Pia, unaweza kutumia sahani za

kawaida unazotumia nyumbani kuwawekea

vifaranga chakula.

_Hapa inategemea na jinsi ulivyo jipanga unaweza kununua vyombo vya chakula au ukatengeneza mwenyewe kwa kutumia mbao, dumu nk. (Zingatia usafi)

_Kitu cha kufahamu ni kuwa vyombo vya chakula ndio vinahitajika kuwa vingi kuliko vyombo vya maji.

_Vifaranga utakapo wawekea chakula wengi watakimbilia kula na wakati wa kunywa maji Vifaranga wataenda wachache wachache, hivyo vyombo  vya chakula vikiwa vichache kuna urahisi vifaranga wengine wakakosa kula,wakapigana,kudonoana na mwisho wa siku kuna baadhi ya Vifaranga vitakuwa dhaifu na hata maumbo yao yatakuwa madogo kuliko wenzao kwaajili ya kukosa chakula (vitadumaa).

3. Vyombo Vya Maji

Chombo chochote chenye kina kifupi kinafaa kwa

kuwayweshea kuku ila budi kiinuliwe ili vifaranga wasiweze kuingiza takataka za chini kwenye maji. Pia kama ni cha wazi sehemu ya kunywea maji pawekewe changarawe safi kabisa ili kuzuia vifaranga wasiloane maji wakati wanapo kunywa.

“Najua wengi imewatokea na Vifaranga kufa hasa siku za mwanzo kwaajili ya kulowana maji”

Au tumia sahani na makopokama ifuatavyo.

Toboa sentimita tatu kutoka kwenye mdomo wa kopo, jaza maji katika kopo halafu lifunike kwa sahani na ligeuze.

****************************************************************

Share Now

Related posts